Serikali Wilayani Masasi leo tarehe 08/05/2024 imetoa bati 86, boriti 97, misumari kg 40, saruji mifuko 10, na chakula kwa familia zilizopatwa na maafa ya mvua iliyoambatana na upepo mkali na kusababisha baadhi ya familia kukosa makazi, mvua iliyonyesha siku ya tarehe 01/01/ 2024 majira ya saa 2:00 usiku.
Tukio hilo limetokea Katika Kijiji Cha Mtengula, kata ya Mijelejele Halmashauri ya Wilaya Masasi Mkoani Mtwara.
Akigawa vifaa hivyo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe.Lauter Kanoni, Afisa Tarafa ya Chiungutwa Bw. Ali Kuchele amesema kwamba kufuatia tathimini iliyofanywa na timu ya Wataalamu Kutoka ngazi ya Halmashauri ilibaini uwepo wa uharibifu wa aina mbili, kwanza uharibifu wa makazi, na uharibifu maeneo ya biashara ambapo katika Eneo la Mijelejele walipatikana watu 17 na katika Kata ya Chiungutwa zilipatikana kaya 146, lakini kwavile kilichopatikana hakiwezi kuwatosheleza watu wote,na ndipo wakaamua kwa kuanzia wapewe kipaunbele wale wote ambao wamekosa makazi moja kwa Moja na wapo katika hali mbaya zaidi.
Amesema "mnamo Siku ya tarehe 01/01/2024 katika eneo la Wilaya yetu ya Masasi ilijitokeza maafa ya mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali na maeneo yaliyokuwa yameathirika zaidi ni mawili kata ya Mijelejele na Kata ya Chiungutwa ambapo kwa jitihada kubwa zilizofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Masasi kuwatafuta wadau mbalimbali ili kuweza kupata chochote kitu (msaada) ili kuwashika mkono ndugu zetu na baada ya hapo mkuu wa Wilaya aliweza kufanya Uzinduzi wa ugawaji wa vifaa hivyo katika Tarafa ya Chiungutwa kwani jumla ya shilingi milioni 22,600,000 zimetolewa kwaajili ya kuwashika mkono waathirika hao"...... alisema Bw. Kuchele.
Ameongeza kuwa" Mkuu wa Wilaya ametoa salamu hizi za pole kwenu na pia anawashukuru kwa ustahamilivu wenu tangu mlipopata maafa hayo na pia tunawashukuru sana watu wengine pamoja na ndugu zenu kwa kuwapa msaada wa makazi kwa muda."
Naye Diwani wa kata hiyo ya Mijelejele mhe. Juma Pole pamoja na kuendelea kuwapa pole kwa maafa hayo pia ametumia nafasi hiyo kuwaeleza wananchi hao kuwa, Serikali ya awamu ya 6 inawapenda sana kwasababu maafa hayo ya tarehe mosi hayajaigusa Mijelejele peke yake bali ni maafa ambayo yametokea maeneo mengi katika Eneo la Masasi, katika Mkoa na Tanzania kwa ujumla hivyo yawapasa kumuombea dua njema mhe. mkuu wa Wilaya ya Masasi Lauter Kanoni kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kwenye Wilaya ya Masasi sanjari na msaada huu ambao Leo wana Mijelejele wameupata.
Amesema vifaa hivi hawawezi kupata watu wote isipokuwa wanatakiwa kushukuru kwa kile walichokipata kwani Serikali haiwezi kumaliza kila kitu bali inakuja kuchochea pale ambapo wao wanapaswa waanze kufanya.
Mzee chifu Magambo pamoja Naye Bw. Ali Bakari ambaye ni Imamu wa msikiti wa Mtengula, Hawa ni miongoni mwa walengwa waliopata msaada huo wote kwa Pamoja wamewashukuru viongozi wote ambao wameungana na kufanikisha wao kupatiwa misaada hiyo ambayo ilikuwa ikifanyika katika maeneo mengine Lakini Leo na wao wamepatiwa .
Imeandaliwa na Winifrida Ndunguru,
...............Afisa Habari MDC
Masasi - Bomani
Anuani ya Posta: S.L.P 60 Masasi
Simu ya mezani: 023-2510031
Simu ya kiganjani: 023-2510031
Baruapepe za Watumishi: ded@masasidc.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Haki Zote Zimehifadhiwa